Mtukuze Mungu katika Mwili Wako
- Dalvin Mwamakula
- May 29
- 2 min read

Ulinunuliwa kwa gharama kubwa. Kwa hiyo mtukuze Mungu katika mwili wako. (1 Wakorintho 6:20)
“Kuabudu” ni neno tunalotumia kuelezea matendo yote ya moyo na akili na mwili ambayo yanadhihirisha kimakusudi thamani ya Mungu isiyo na kikomo. Hivi ndivyo tulivyoumbwa kwa ajili yake. Huenda ikawa ni kuimba kanisani. Inaweza ikawa kufagia sakafu jikoni.
Usifikirie tu kuhusu ibada za kanisani unapofikiria kuhusu kuabudu. Hiko ni kizuizi kikubwa sana ambacho hakipo kwenye Biblia. Maisha yote yanapaswa kuwa ibada.
Chukua kifungua kinywa, kwa mfano, au vitafunio vya asubuhi. 1 Wakorintho 10:31 inasema, "Mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu." Sasa kula na kunywa ni mambo ya msingi ambayo unaweza kuyapata. Je, ni nini kinachoweza kuwa halisi zaidi au zaidi ya kibinadamu kuliko kula na kunywa? Na Paulo asema, kwa kweli, kula na kunywa kwenu vyote na viwe ibada.
Au chukulia kujamiiana. Paulo anasema mbadala wa uasherati ni ibada.
Ikimbieni zinaa. Dhambi nyingine zote anazofanya mtu ni nje ya mwili wake, lakini mwasherati hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, kwa maana mlinunuliwa kwa gharama kubwa. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu. (1 Wakorintho 6:18-20)
Yaani abudu kwa mwili wako kwa jinsi unavyoshughulikia ujinsia wako.
Au chukulia kifo kwa mfano wa mwisho. Tutapata kifo katika miili yetu. Kwa kweli, litakuwa tendo la mwisho la mwili katika dunia hii. Mwili unaaga. Je, tutaabuduje katika tendo hilo la mwisho la mwili? Tunaona jibu katika Wafilipi 1:20–21. Paulo anasema kwamba tumaini lake ni kwamba Kristo atukuzwe - aabudiwe, kuonyeshwa kuwa anastahili - katika mwili wake kwa kifo. Kisha anaongeza, “Kwa maana kwangu mimi . . . kufa ni faida.” Tunadhihirisha thamani isiyo na kikomo ya Kristo katika kufa kwa kuhesabu kifo kama faida.
Unao mwili. Lakini sio wako. “Mlinunuliwa kwa gharama kubwa. Basi mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”
Wewe daima hupo ndani ya hekalu. Abudu kila mara.




Comments