top of page

Mungu Anaudhihirisha Upendo Wake

  • Writer: Dalvin Mwamakula
    Dalvin Mwamakula
  • Apr 28
  • 2 min read

Updated: May 1

Mungu aonyesha [anaudhihirisha] upendo wake kwetu kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. (Warumi 5:8)


Ona kwamba “unaudhihirisha” ni wakati uliopo na “alikufa” ni wakati uliopita. "Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi."

 

Wakati uliopo unamaanisha kuwa huu udhihirisho ni tendo linaloendelea kutokea hata hivi leo. Na litaendelea kutokea kesho.

 

Wakati uliopita "alikufa" inamaanisha kwamba kifo cha Kristo kilitokea mara moja kwa wote na hakitarudiwa. “Kristo pia aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio na haki, ili atulete kwa Mungu” (1 Petro 3:18).

 

Kwa nini Paulo alitumia wakati uliopo (“Mungu anadhihirisha”)? Ningelitarajia Paulo aseme, “Mungu alidhihirisha (wakati uliopita) pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Je, kifo cha Kristo kilipotukia hakikuwa udhihirisho wa upendo wa Mungu? Na je, udhihirisho huo haukufanyika wakati uliotipa?

 

Nadhani kidokezo kimetolewa aya chache nyuma kidogo. Paulo amesema hivi punde kwamba “mateso huleta saburi, na saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini, na tumaini halitukatishi tamaa” (Warumi 5:3–5).

 

Kwa maneno mengine, lengo la kila jambo ambalo Mungu anatupitisha ni tumaini. Anataka tuwe na tumaini lisiloyumbayumba katika dhiki zote.

 

Lakini tunawezaje?

 

Paulo anajibu katika mstari unaofuata: “Kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Warumi 5:5). Upendo wa Mungu umemiminwa ndani ya mioyo yetu. Hali ya kitenzi hiki ina maana kwamba upendo wa Mungu ulimiminwa mioyoni mwetu hapo awali (wakati wa kuongoka kwetu) na bado upo na unatenda kazi.

 

Mungu anadhihirisha upendo wake kwetu kwa kumtoa Mwana wake mwenyewe afe mara moja tu wakati uliopita kwa ajili ya dhambi zetu (Warumi 5:8). Lakini pia anajua kwamba upendo huu wa zamani lazima uonekane kama ukweli wa sasa (leo na kesho) ikiwa tunataka kuwa na uvumilivu na tabia na matumaini.

 

Kwa hiyo, hakuudhihirisha pale Kalvari pekee; anaendelea kuudhihirisha sasa kwa Roho ndani ya mioyo yetu. Anafanya hivyo kwa kufungua macho ya mioyo yetu ili kuonja na kuona utukufu wa msalaba na hakikisho unaotoa kwamba hakuna kitu kinachoweza kututenganisha na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu (Warumi 8:38-39).

Comments


100Fold Logo

NJIA ZA KUTUFUATILIA

  • Youtube
  • WhatsApp
  • Email
  • Facebook
  • Instagram
bottom of page