Upendo Mkuu
- Dalvin Mwamakula
- Jan 27
- 2 min read

Ninawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu kwa ajili ya jina lake. (1 Yohana 2:12)
Kwa nini tunapaswa kusisitiza kwamba Mungu anapenda, anasamehe, na anaokoa “kwa ajili ya jina lake”— kwa ajili ya utukufu wake? Hapa kuna sababu mbili (kati ya nyingi).
1) Tunapaswa kusisitiza kwamba Mungu anapenda na kusamehe kwa ajili ya utukufu wake mwenyewe kwa sababu Biblia hufanya hivyo.
Mimi, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. (Isaya 43:25)
Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu, unisamehe kosa langu, maana ni kubwa. (Zaburi 25:11)
Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetukwa ajili ya jina lako. (Zaburi 79:9)
Ingawa dhambi zetu zinashuhudia juu yetu, Ee Bwana, tenda jambo kwa ajili ya jina lako. (Yeremia 14:7)
Tunakiri uovu wetu, ee Mwenyezi-Mungu, na uovu wa baba zetu, kwa kuwa tumekutenda dhambi. Usitudharau, kwa ajili ya jina lako; usikivunjie heshima kiti chako cha enzi kitukufu.(Yeremia 14:20-21)
Yeye [Kristo] ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu. (Warumi 3:25-26)
Umesamehewa dhambi zako kwa ajili ya jina lake. (1 Yohana 2:12)
Mungu anatupenda kwa kutuonyesha ukuu wake, si kwa kutufanya kuwa wakuu. Kufika mbinguni na kujiona sisi wenyewe kuwa wakuu ingekuwa huzuni kuu.
2) Tunapaswa kusisitiza kwamba Mungu anapenda na kusamehe kwa ajili ya utukufu wake mwenyewe kwa sababu inaweka wazi kwamba Mungu anatupenda kwa upendo mkuu zaidi.
Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami mahali nilipo, wauone utukufu wangu. (Yohana 17:24)
Mungu anatupenda sio kwa njia inayotufanya kuwa na ukuu zaidi, bali anajifanya yeye mwenyewe kuwa mkuu zaidi. Mbingu haitakuwa ukumbi wa vioo - vya kujiangalia sisi wenyewe, lakini maono yanayoongezeka ya ukuu usio na mwisho. Kufika mbinguni na kugundua kwamba sisi ni wakuu ingekuwa huzuni kuu.
Upendo mkuu zaidi huhakikisha kwamba Mungu anafanya kila jambo kwa njia ya kutegemeza na kutukuza ukuu wake mwenyewe ili kwamba, tunapofika mbinguni, tuwe na kitu cha kuongeza shangwe yetu milele: utukufu wa Mungu. Upendo mkuu zaidi ni Mungu kujitoa kwetu kwa ajili ya furaha yetu ya milele, kwa gharama ya maisha ya Mwana wake (Warumi 8:32). Hicho ndicho anachomaanisha anaposema kwamba anatupenda na kutusamehe kwa ajili ya jina lake mwenyewe.
Upendo mkuu ni Mungu kuutukuza ukuu wake, ili tuwe na shangwe ya milele kwa utukufu wake, akijitoa kwetu kwa furaha yetu ya milele kwa gharama ya Mwana wake, akitupenda na kutusamehe kwa ajili ya jina lake.




Comments