Vitabu Vitavyosomwa katika Hukumu
- Dalvin Mwamakula
- Mar 31
- 2 min read

Nao wote waishio duniani watamwabudu huyo mnyama, yaani, wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. (Ufunuo 13:8)
Wokovu umehakikishwa kwa wote walioandikwa katika kitabu cha uzima.
Sababu ya kuandikwa katika kitabu cha uzima kunatuhakikishia wokovu ni kwamba kitabu hicho kinaitwa “kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa. Majina katika kitabu hiki hayajahifadhiwa kwa misingi ya matendo yao. Wanaokolewa kwa msingi wa kifo cha Kristo.
Lakini Yohana asema katika Ufunuo 20:12, “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Kisha kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni kitabu cha uzima. Na wafu wakahukumiwa katika yale yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” Kwa hivyo, ni jinsi gani basi rekodi ya maisha yetu iliyomo katika “vitabu” ina sehemu katika hukumu yetu, ikiwa tunaokolewa kwa msingi wa kifo cha Kristo?
Jibu ni kwamba vitabu, vinavyorekodi matendo yetu, vina ushahidi wa kutosha wa sisi kuwa mali ya Kristo kiasi kwamba vinafanya kazi kama uthibitisho wa hadharani wa imani yetu na muungano wetu pamoja na Kristo.
Fikiria andiko la Ufunuo 21:27: “Hakuna kitu kilicho najisi kitakachoingia [Yerusalemu mpya] kamwe, wala yeyote afanyaye mambo ya kuchukiza au ya uongo, bali wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.” Hapa matokeo ya kuandikwa katika "kitabu cha uzima" sio tu kutokuangamia, lakini pia sio kufanya mambo ya kuchukiza, ya tabia za dhambi.
Kwa mfano, fikiria mwizi aliyekuwa msalabani. Yesu alisema kwamba ataingia paradiso (Luka 23:43). Lakini hukumu itakuwaje kwake vitabu vitakapofunguliwa? Zaidi ya 99.9% ya maisha yake itakuwa dhambi.
Wokovu wake utahakikishwa kwa damu ya Kristo. Jina lake litakuwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyekufa.
Kisha Mungu atafungua vitabu. Kwanza, atatumia rekodi ya maisha yote ya dhambi kumtukuza Mwanae ambaye ni dhabihu kuu. Na, pili, Mungu atasoma ukurasa wa mwisho, ambapo mabadiliko makubwa ya mwizi msalabani yameandikwa. Kazi hii ya Mungu katika maisha yake, iliyorekodiwa katika vitabu, kuhusu siku hiyo ya mwisho itakuwa uthibitisho wa hadharani wa imani ya mwizi na muungano wake na Kristo. Na Kristo atakuwa msingi wa wokovu wake, sio matendo yake.
Kwa hiyo, ninaposema kwamba yaliyoandikwa katika vitabu ni uthibitisho wa hadharani wa imani yetu na muungano na Kristo, simaanishi kwamba rekodi itakuwa na matendo mema zaidi kuliko mabaya.
Ninamaanisha kwamba kutaandikwa pale aina ya maisha katika Kristo ambayo yanaonyesha ukweli wa imani - ukweli wa kuzaliwa upya na kuunganishwa pamoja na Kristo. Hivyo ndivyo tunavyoianza kila siku kama Mkristo: tukiwa na ujasiri kwamba hukumu yetu imepita (Warumi 8:1), na kwamba jina letu limo katika kitabu cha uzima, na kwamba yeye aliyeanza kazi njema ndani yetu ataileta katika ukamilifu katika ile siku ya Kristo.
Comments