Chochote Ambacho Hakitokani Na Imani Ni Dhambi — Kweli?
- Dalvin Mwamakula
- Feb 4
- 4 min read


Makala imeandwika na John Piper
Mwanzilishi na Mwalimu, desiringGod.org
Tangu wakati wa John Chrysostom (347–407) watu wamejaribu kupunguza maana ya maneno ya Paulo katika Warumi 14:23, “Chochote kisichotokana na imani ni dhambi.” Chrysostom anaonya, “Sasa mambo haya yote yamesemwa na Paulo kuhusu mada iliyopo, si kuhusu kila kitu.”
Leon Morris anaendeleza kizuizi hiki na kusema,
Lolote liwe kweli kuhusu matendo yaliyofanyika kabla ya mtu kuwa muumini, Paulo hayajadili hapa. Kujali kwake kunahusu hasa muumini ambaye wakati mwingine hufanya mambo ambayo hayachochewi na imani. (Waraka kwa Warumi, 493)
Lakini Richard Lenski anasema, Hapana!
Je, hili linapaswa kuzuiliwa kwa Mkristo pekee na kwa suala la adiaphora [mambo yasiyo ya lazima kwa imani], yaani, kwa imani ndani ya uwanja huu? Hapana; inashughulikia eneo hili tu kwa sababu ni sehemu ya eneo kubwa zaidi. (Ufafanuzi wa Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Warumi, 854)
Unafikiri nini?
Huu hapa ni muktadha wa kukusaidia kupata mwelekeo (Warumi 14:21–23):
Ni vizuri kutokula nyama au kunywa divai au kufanya jambo lolote linalomkwaza ndugu yako. Imani uliyonayo, iwe kati yako na Mungu. Heri mtu yule ambaye hana sababu ya kujihukumu kwa kile anachokubali. Lakini yeyote anayekuwa na shaka anahukumiwa akila, kwa sababu kula kwake hakutokani na imani. Kwa maana lolote lisilotokana na imani ni dhambi.
Augustino, katika Mihadhara yake juu ya Injili kulingana na Mtakatifu Yohana, ananukuu Warumi 14:23 kama tamko la jumla linalohusu hali zote za kibinadamu:
Si kwamba unaweza kusema, “Kabla ya kuamini nilikuwa tayari nafanya matendo mema, na kwa hiyo nilichaguliwa.” Kwa kazi gani nzuri inaweza kuwa kabla ya imani, wakati mtume anasema, “Chochote kisicho tokana na imani ni dhambi”? (Nicene and Post-Nicene Fathers, Toleo la 7)
Thomas Schreiner anakubaliana na Augustine na anaeleza kwamba Paulo angeweza kutoa hoja ndogo zaidi kwa kusimama na sehemu ya kwanza ya mstari wa 23 (“Lakini yeyote anayekuwa na shaka anahukumiwa ikiwa anakula, kwa sababu kula hakutokani na imani”). Hoja imetolewa. Mwisho wa hoja. Lakini hapana. Sasa anaongeza kauli isiyo na masharti, “Kwa maana chochote kisicho tokana na imani ni dhambi” (Warumi , 739).
Msaada wa Ulimwengu kwa Hoja Mahususi
Ni kweli, kama Morris anavyosema, kwamba Paulo hazungumzii matendo ya wasioamini katika Warumi 14. Lakini hiyo si hoja yenye nguvu. Mara kwa mara tunaunga mkono hoja mahususi kwa hoja za jumla.
"Wema" wote wa mwanadamu umepotoka ikiwa hautokani na moyo wa upendo kwa Baba wa mbinguni — hata kama tabia inalingana na kanuni za kibiblia.
Kwa mfano, tunaweza kusema, “Mikono mirefu ya saa za zamani katika duka hili huzunguka nyuzi 360 kila saa.” Kwa sababu mikono mirefu ya saa zote zenye nyuso za mviringo huzunguka nyuzi 360 kila saa. Hakuna mtu angeona sisi kuwa na utimamu wa akili tukisema, “Kutokana na sentensi hizi mbili, tunachoweza kujifunza ni kwamba saa pekee ambazo mikono mirefu huzunguka nyuzi 360 kila saa ni saa za zamani katika duka hili, kwa sababu hizo ndizo tunazozungumzia.” Hapana. Tulileta hoja ya jumla ili kuunga mkono ile mahususi.
Hivyo ndivyo Paulo alivyofanya. “Chochote kisichotokana na imani ni dhambi” ni hoja ya jumla. Hili linainngwa mkono mara nyingi nje ya Warumi 14:23. Kwa mfano:
1. Jambo la Paulo katika Warumi 4:20 ni kwamba imani inamtukuza Mungu: “Abrahamu akaimarika katika imani yake akimtukuza Mungu.” Sababu ya matendo yasiyo na imani kuwa dhambi ni kwamba hayamtukuzi Mungu kama mwaminifu.
2. Katika 1 Wakorintho 10:31, Paulo alisema, “Lolote mfanyalo, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” Lakini huwezi kumtukuza Mungu ikiwa unamdharau kwa kutomwamini. Kwa hiyo, pale ambapo hakuna imani, 1 Wakorintho 10:31 inakiukwa katika kila tendo (bila kujali jinsi lilivyo lenyewe kwa asili).
3. Waebrania 11:6 inasema, “Bila imani haiwezekani kumpendeza.” Kwa hiyo, pale ambapo hakuna imani, matendo yote hayampendezi Mungu.
Wakati Wema Unapokuwa Dhambi
Ndio maana Augustino alisema hata wema wa wasioamini ni dhambi. Mfano unaweza kufanya shutuma hii kali ya “wema” wa kibinadamu usio na imani kuwa wazi zaidi.
Fikiria wewe ni baba wa kijana wa umri wa balehe. Unamkumbusha kuosha gari kabla hajaitumia kuwapeleka marafiki zake kwenye mchezo wa mpira wa kikapu baadaye leo usiku. Hapo awali alikubali kufanya hivyo.
Ana kasirika na kusema hataki. Unamkumbusha kwa upole lakini kwa uthabiti ahadi yake, na kusema ndivyo unavyotarajia. Anapinga. Unasema, “Basi, kama utatumia gari usiku wa leo, hivyo ndivyo ulivyo kubaliana na mimi kufanya.” Anatoka nje ya chumba kwa hasira. Baadaye unamwona anaosha gari.
Upotovu wetu ni hali katika uhusiano na Mungu kimsingi, na pili tu katika uhusiano na mwanadamu.
Lakini hafanyi hivyo kwa ajili ya upendo kwako au kwa tamaa ya kumheshimu Kristo kwa kutii Maandiko. Anataka kwenda kwenye mchezo na marafiki zake. Hicho ndicho kinachoulazimisha "utii" wake. Ninaweka “utii” katika nukuu kwa sababu ni wa nje tu. Moyo wake hauko sahihi. Hiki ndicho ninachomaanisha ninaposema kwamba “wema” wote wa kibinadamu umepotoka ikiwa hautokani na moyo wa upendo kwa Baba wa mbinguni — hata kama tabia hiyo inaendana na kanuni za Biblia.
Kwanza kabisa kwa Mungu
Hali ya kutisha ya moyo wa mwanadamu haitatambuliwa kamwe na watu wanaoitathmini tu kuhusanisna na watu wengine. Mwanao atawapeleka marafiki zake kwenye mchezo wa mpira. Hiyo ni "fadhili." Wataipokea kama "faida." Kwa hiyo, uovu wa matendo yetu hauwezi kupimwa tu kwa wema au madhara wanayopata wanadamu wengine.
Warumi 14:23 inaweka wazi kwamba upotovu wetu ni hali katika uhusiano na Mungu kimsingi, na pili tu katika uhusiano na mwanadamu. Huu ndio uamsho mkubwa unaohitajika kutokea ili watu waone ukubwa wa dhambi zao na ukuu wa Mwokozi.
Comments