Sababu Kumi za Kukariri Sehemu Kubwa za Biblia
- Dalvin Mwamakula
- Apr 3
- 4 min read


Makala imeandwika na Jon Bloom
Mwandishi mfanyakazi, desiringGod.org
Unaweza kukariri sehemu kubwa, hata vitabu vizima vya Biblia. Isipokuwa kama wewe ni sehemu ya asilimia ndogo sana kati yetu ambao wanakabiliwa na jeraha la ubongo au kiharusi au ulemavu, unaweza kweli. Na unapaswa kufanya hivyo. Lakini kwa nini?
1. Kwa sababu una kumbukumbu mbaya.
Usiseme huwezi kukariri kwa sababu una kumbukumbu mbaya. Hiyo ndiyo sababu unahitaji kukariri. Nina kumbukumbu mbaya pia. Nadhani ni mbaya kuliko wastani — kwa kweli. Ninasahau majina ya watu ninaowajua na kuwaona mara kwa mara! Lazima nilazimishe akili yangu yenye mapungufu na isiyo na ufanisi kuhifadhi mambo ya muhimu zaidi kwenye kumbukumbu ya muda mrefu. Hii hutokea tu kwa mchakato wa kurudia (kukariri) kila siku kwa muda fulani. Utashangaa ni mambo gani unaweza kukumbuka ikiwa una mfumo rahisi na ukiweka juhudi kidogo. Nimekariri vitabu vitano vya Agano Jipya na ninafanyia kazi kitabu changu cha sita. Na hiyo ni kwa sababu nina kumbukumbu mbaya.
2. Kwa sababu unahitaji kuilisha akili yako.
Wafilipi 4:8 inatuambia tufikirie juu ya chochote ambacho ni cha kweli, chenye heshima, haki, safi, chenye kupendeza, kinachostahili sifa, bora, na kinachostahili kusifiwa. Lakini tunawezaje kufanya hivyo ikiwa hatuwezi kukumbuka mambo kama hayo? Mawazo chanya ya jumla ya Biblia hayasaidii sana. Tunahitaji "ahadi za thamani na kubwa sana" maalum katika kumbukumbu zetu ili kuvuta tunapokuwa peke yetu na kupigana na kuvunjika moyo au hasira au tamaa au hofu (2 Petro 1: 4).
3. Kwa sababu Biblia inapatikana kiurahisi sana kwako.
Inashangaza jinsi gani kuwa na wingi wa kitu kunaweza kusababisha kukipuuza. Ikiwa Biblia iko kila wakati kwenye meza, simu, na kompyuta zetu, tunaweza kuisoma kidogo kidogo, kusoma sehemu, na kutafuta maneno muhimu tunapohitaji, lakini hatuhisi haraka ya kuielewa kwa undani. Kukariri ni njia mojawapo ya kupambana na udanganyifu huo.
4. Kwa sababu una Mtandao [Intaneti].
Kwa bahati mbaya, Intaneti inatufundisha jinsi ya kutosoma. Tunakuwa wachunguzi wa taarifa kwa juu juu tu, tunapitia haraka lakini hatumeng'enyi taarifa, hatuielewi sana. Tunapoteza uvumilivu kwa usomaji wa kina na wa kutafakari zaidi. Kukariri vifungu virefu vya Maandiko hutulazimisha kutafakari kwa kina maana na matumizi.
5. Kwa sababu huijui Biblia vizuri kama unavyofikiri unaijua.
Umewahi kuwa na mazungumzo na rafiki ambaye umemjua kwa muda mrefu na kugundua kuwa kuna mambo kumhusu ambayo hukuyajua, na ghafla ukamwelewa vizuri zaidi na kuhisi ukaribu naye? Hivyo ndivyo kukariri vifungu virefu na hata vitabu vya Biblia vitakavyokufanyia. Utapata marafiki wazuri kwenye Biblia watakaokuwa wasiri na washauri wa dhati.
6. Kwa sababu neno la Mungu litakuwa la thamani zaidi kwako.
Vitu tunavyowekeza zaidi ndani yake vinakuwa vya thamani zaidi kwetu. Iwapo utatumia muda kidogo tu kusoma Biblia, usitarajie iwe ya thamani kwako. Lakini ikiwa utatumia mamia ya masaa kuhifadhi sehemu kubwa za neno la Mungu moyoni mwako ili neno la Kristo likae ndani yako kwa wingi, litakuwa sehemu ya thamani ya maisha yako muhimu (Zaburi 119:11; Wakolosai 3:16; Kumbukumbu la Torati 32:47).
Kukariri Maandiko sio ngumu kama unavyofikiri, ni uwekezaji bora wa maisha yako kwa sababu hizi kumi. Hutajutia kamwe.
7. Kwa sababu utauona utukufu wa Mungu zaidi.
Tunaweza kujua mambo machache tu kuhusu mtu kwa kile anachotengeneza. Tunaweza kuwajua vyema kwa yale wanayosema. Milima na vijidudu, galaksi na mbuzi, kila kimoja kinasema mambo mazuri kuhusu Mungu. Lakini kumjua Mungu kweli kweli, kuona na kustaajabu mambo ambayo ni ya utukufu zaidi juu yake, ni lazima tusikilize kwa makini kile anachosema juu yake mwenyewe, kwa sababu Mungu hujidhihirisha hasa kwa neno lake (1 Samweli 3:21). Kuhifadhi neno lake kunatusaidia kusikiliza kwa makini na kuona utukufu zaidi.
8. Kwa sababu itakurekebishia kipimo chako cha kuhisi maneno ya upuuzi.
Dunia inakudanganya wakati wote. Ibilisi ni baba wa uongo (Yohana 8:44), na ulimwengu unakaa katika uwezo wake (1 Yohana 5:19). Na asili yako ya dhambi inakudanganya. Na ndugu wa uongo wanakudanganya. Kadiri unavyojua neno la Mungu vizuri zaidi, ndivyo unavyozidi kuwa na ustadi katika kulishughulikia (2 Timotheo 2:15). Kadiri unavyokuwa na neno lake wazi akilini mwako, ndivyo utakavyoweza kutambua upuuzi wa kishetani kwa usahihi zaidi. Kuwa na neno la Mungu kwa wingi akilini mwako kutarekebisha kipimo chako cha upuuzi.
9. Kwa sababu utateseka.
Mateso yanakuja kwako (au yamefika tayari) na yanachanganya na kupotosha. Kukumbuka sehemu kubwa za Maandiko ni msaada mkubwa sana kwenye nyakati kama hizi. Siyo tu kwamba utakuwa na maandiko mahususi yanayokujia akilini, lakini hata wakati ambapo, kutokana na maumivu au hofu, unapata shida kuyakumbuka, utajua wapi pa kwenda. Kukariri vitabu kunachapisha vitabu hivyo akilini mwako. Utajua ni sura na sehemu zipi zitazungumza juu ya mateso yako.
10. Kwa sababu ndugu zako watateseka.
Hali ni hiyo hiyo kweli kwa kuleta faraja na ushauri wa injili kwa ndugu yako au dada yako anayeteseka. Kukariri sehemu kubwa ya maandiko haikusaidii wewe pekee, bali pia ni njia ya kuwapenda wengine kwa kuwa na uwezo wa kuwapa ukweli unaodumisha imani wakati ambapo unahitajika zaidi.
Jinsi ya Kukariri Sehemu Ndefu za Maandiko
Pitia, Soma, Kariri, Rudia
Unafanya mstari mmoja au miwili kwa wakati mmoja. John Piper na mimi, pamoja na wengine kadhaa, tunatumia mbinu rahisi sana ambayo Andrew Davis alianzisha. Hebu tutumie Yohana 1:1–3 kama mfano.
[1]Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
[2]Yeye hapo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
[3]Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
Siku ya 1:
Soma Yohana 1:1 mara kumi (isome kila mara ili kuyaweka maneno akilini mwako).
Kisha ifunge Biblia yako na urudie bila kusoma mara kumi (nashauri ufanye kwa sauti).
Siku ya 2:
Pitia upya Yohana 1:1 kisha urudie na kukariri mara kumi kwa kumbukumbu.
Soma Yohana 1:2 mara kumi.
Funga Biblia yako na urudie kwa sauti mara kumi.
Siku ya 3:
Soma Yohana 1:1 mara moja kwa kumbukumbu.
Rudia Yohana 1:2 mara kumi kwa kumbukumbu.
Soma Yohana 1:3 mara kumi.
Funga Biblia yako na rudia kwa sauti mara kumi.
Na kuendelea na kuendelea. Pitia, soma, kariri, rudia. Ikiwa unarudia mstari kwa kumbukumbu mara moja kwa siku kwa siku mia moja, itakuwa katika kumbukumbu yako ya kudumu ya muda mrefu.
Ikiwa unataka kujua jinsi ya kuendeleza tabia ya kupitia kusoma, Andrew Davis ana kitabu cha kurasa 30 cha jinsi ya kufanya hivi ($0.99 ~Tsh2,500/- pekee kwenye Kindle!).
Unaweza kufanya hivi! Unaweza hakika! Na unapaswa. Kukariri sehemu kubwa za Maandiko sio ngumu kama unavyofikiri na itakuwa moja ya uwekezaji bora wa maisha yako kwa sababu kumi zilizoorodheshwa hapo juu na zaidi. Hutajutia kamwe.
Kommentare